Utajiri

Biblia inatoa mtazamo wenye uwiano juu ya mali: Mungu anaweza kubariki kwa utajiri, lakini inaonya juu ya hatari zake, ikisisitiza kwamba utajiri wa kweli ni uhusiano naye. Mali ni ya muda, haiwezi kununua wokovu, na inaweza kuleta kiburi, utengano na kutozaa matunda kiroho.

Mtazamo wa Biblia juu ya mali

Mtazamo wa Bwana juu ya utajiri

Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani. (Ufunuo 2:9)

Mtazamo wa watu juu ya mali

Wenye njaa huyala mavuno yake, wakiyatoa hata katikati ya miiba, nao wenye kiu huitamani sana mali yake. (Ayubu 5:5)
Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu, wala mali zake hazitakuwa nyingi juu ya nchi. (Ayubu 15:29)
Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini, nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyangʼanya watu. (Ayubu 20:10)
Atatema mali alizozimeza; Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika. (Ayubu 20:15)
Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila; hatafurahia faida itokanayo na biashara yake. Kwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu; amenyangʼanya kwa nguvu nyumba asizozijenga. “Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana; hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake. (Ayubu 20:18-20)
...giza nene linavizia hazina zake. Moto usiopepewa na mtu utamteketeza, na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake. (Ayubu 20:26)
Mafuriko yataichukua nyumba yake, maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu. (Ayubu 20:28)
Huitumia miaka yao katika mafanikio nao hushuka kaburini kwa amani. (Ayubu 21:13)
Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe, hivyo najitenga mbali na shauri la waovu. (Ayubu 21:16)
Kama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya: Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako, kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi, dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni, ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako, naye atakuwa fedha yako iliyo bora. (Ayubu 22:23-25)
“Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu, urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi: (Ayubu 27:13)
Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi, na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi, yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa, naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake. (Ayubu 27:16-17)
Kama wakitii na kumtumikia, wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio, na miaka yao katika utoshelevu. (Ayubu 36:11)
Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki? (Ayubu 36:19)
Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema na huwafaidia wale walionalo jua. Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi, lakini faida ya maarifa ni hii: kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo. (Mhubiri 7:11-12)

Hatuchukui chochote tunapokufa

Usitishwe mtu anapotajirika, fahari ya nyumba yake inapoongezeka, kwa maana hatachukua chochote atakapokufa, fahari yake haitashuka pamoja naye. Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri, na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa, atajiunga na kizazi cha baba zake, ambao hawataona kamwe nuru ya uzima. Mwanadamu mwenye utajiri bila ufahamu ni kama wanyama waangamiao. (Zaburi 49:16-20)
Nimeshaona uovu mzito chini ya jua: Utajiri uliolimbikizwa kwa kujinyima na kuleta madhara kwa mwenye mali, au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya, hivyo kwamba wakati akiwa na mwana hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake. Mtu hutoka tumboni mwa mama yake uchi, naye jinsi alivyokuja vivyo hivyo huondoka. Hachukui chochote kutokana na kazi yake ambacho anaweza kukibeba mkononi mwake. (Mhubiri 5:13-15)
Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. (1 Timotheo 6:7)
Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayeifaidi. (Zaburi 39:6)

Huwezi kununua ukombozi wa nafsi yako

Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja, wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka, wale wanaotegemea mali zao na kujivunia utajiri wao mwingi? Hakuna mwanadamu awaye yote awezaye kuukomboa uhai wa mwingine, au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake. Fidia ya uhai ni gharama kubwa, hakuna malipo yoyote yanayotosha, (Zaburi 49:5-8)
Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu, bali haki huokoa kutoka mautini. (Mithali 11:4)
Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? (Mathayo 16:26)
Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? (Marko 8:36-37)
Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake? (Luka 9:25)

Utajiri huleta “marafiki” wengi

Maskini huepukwa hata na majirani zao, bali matajiri wana marafiki wengi. (Mithali 14:20)
Mali huleta marafiki wengi, bali rafiki wa mtu maskini humwacha. (Mithali 19:4)

Utajiri hupita upesi

Usijitaabishe ili kuupata utajiri, uwe na hekima kuonyesha kujizuia. Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka, huwa kama umepata mabawa ghafula, ukaruka na kutoweka angani kama tai. (Mithali 23:4-5)
Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. (Waebrania 11:24-26)
Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. (1 Petro 1:7)
Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, (1 Petro 1:18)

Mali zote si kitu ukilinganisha na kumjua Yesu

Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. (Wafilipi 3:7-8)

Utajiri hauna uhakika

Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. (1 Timotheo 6:17)

Utajiri hauna faida bila Bwana

Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike na watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia. Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima. Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani, hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu. Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote, hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote. Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo mikono yangu ilikuwa imefanya na yale niliyotaabika kukamilisha, kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua. (Mhubiri 2:4-11)

Mambo yenye thamani kuliko utajiri

Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote, wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha. Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri, kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa. Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu. Marijani na yaspi hazistahili kutajwa; thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu. Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi. (Ayubu 28:15-19)
Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali wa waovu wengi; (Zaburi 37:16)
Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi. (Zaburi 119:14)
Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu. (Zaburi 119:72)
Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu, naam, zaidi ya dhahabu safi, (Zaburi 119:127)
Heri mtu yule aonaye hekima, mtu yule apataye ufahamu, kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi. Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye. Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima. (Mithali 3:13-16)
Chagua mafundisho yangu badala ya fedha, maarifa badala ya dhahabu safi, kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye. (Mithali 8:10-11)
Utajiri na heshima viko kwangu, utajiri udumuo na mafanikio. Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi; kile nitoacho hupita fedha iliyo bora. Natembea katika njia ya unyofu katika mapito ya haki, nawapa utajiri wale wanipendao na kuzijaza hazina zao. (Mithali 8:18-21)
Afadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Bwana, kuliko mali nyingi pamoja na ghasia. (Mithali 15:16)
Afadhali kitu kidogo pamoja na haki kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu. (Mithali 16:8)
Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu, kuchagua ufahamu kuliko fedha! (Mithali 16:16)
Ni afadhali kuwa mnyenyekevu katika roho miongoni mwa walioonewa kuliko kugawana nyara pamoja na wenye kiburi. (Mithali 16:19)
Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka. (Mithali 19:1)
Dhahabu kunayo, na marijani kwa wingi, lakini midomo inenayo maarifa ni kito cha thamani kilicho adimu. (Mithali 20:15)
Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi, kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu. (Mithali 22:1)
Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu. (Mithali 28:6)

Aliyepewa vingi atadaiwa vingi

Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi. (Luka 12:48)

Baraka za utajiri

Wenye haki watazawadiwa mafanikio

Balaa humwandama mtenda dhambi, bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki. (Mithali 13:21)
Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa, bali mapato ya waovu huwaletea taabu. (Mithali 15:6)

Utajiri kwa mtu anayelitafakari Neno la Mungu

Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha. Bali huifurahia sheria ya Bwana, naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana. Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa. (Zaburi 1:1-3)

Waliofanikiwa watamwabudu Bwana

Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu. Wote waendao mavumbini watapiga magoti mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. (Zaburi 22:29)

Kuombea mafanikio

...ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako, niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako, na kuungana na urithi wako katika kukusifu. (Zaburi 106:5)
Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu: “Wote wakupendao na wawe salama. Amani na iwepo ndani ya kuta zako na usalama ndani ya ngome zako.” (Zaburi 122:6-7)
Bwana na akubariki kutoka Sayuni siku zote za maisha yako, na uone mafanikio ya Yerusalemu, (Zaburi 128:5)
Mpendwa, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya njema kama vile roho yako ifanikiwavyo. (3 Yohana 2)

Watu matajiri wanaomcha Mungu

Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Loti mwana wa ndugu yake, mali zote walizokuwa nazo pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri mpaka nchi ya Kanaani, wakafika huko. (Mwanzo 12:5)
Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu. (Mwanzo 13:2)
Kisha Bwana akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. (Mwanzo 15:13-14)
Wakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye Bwana alikuwa amembariki katika kila njia. (Mwanzo 24:1)
Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mtu aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake akapanda juu. (Mwanzo 24:16)
Bwana amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda. (Mwanzo 24:35)
Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. (Mwanzo 26:12-14)
Kwa njia hii Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, watumishi wa kike na wa kiume na ngamia na punda. (Mwanzo 30:43)
Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea. (Mwanzo 33:11)
Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. (Mwanzo 41:42)
Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.” (Mwanzo 45:13)
Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. (Mwanzo 46:6)
Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko wakastawi na kuongezeka kwa wingi sana. (Mwanzo 47:27)
...akisema, “Rudini nyumbani mwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia wingi wa nguo, nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.” (Yoshua 22:8)
Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi. (Ruthu 2:1)
“Enyi binti za Israeli, lieni kwa ajili ya Sauli, ambaye aliwavika nguo nyekundu na maridadi, ambaye aliremba mavazi yenu kwa mapambo ya dhahabu. (2 Samweli 1:24)
Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. (1 Wafalme 10:4, 7)
Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako. Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. (1 Wafalme 3:11-13)
Solomoni akaketi kwenye kiti cha enzi cha Bwana kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana na Israeli wote wakamtii. (1 Nyakati 29:23)
Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Solomoni mwanawe akawa mfalme baada yake. (1 Nyakati 29:28)
Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.” (2 Nyakati 1:11-12)
Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. (2 Nyakati 9:22)
Kwa hiyo Bwana akauimarisha ufalme chini ya uongozi wake, nao Yuda wote wakamletea Yehoshafati zawadi, hivyo akawa na utajiri mwingi na heshima. (2 Nyakati 17:5)
Baadhi ya Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na fedha kama ushuru, nao Waarabu wakamletea mifugo: kondoo dume 7,700 na mbuzi 7,700. Yehoshafati akaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi, akajenga ngome na miji ya hazina katika Yuda (2 Nyakati 17:11-12)
Basi, Yehoshafati alikuwa na mali nyingi sana na heshima. Naye akafanya urafiki na Ahabu kwa mwanawe kumwoa binti wa Ahabu. (2 Nyakati 18:1)
Hezekia alikuwa na utajiri mwingi sana na heshima, naye akajifanyia hazina kwa ajili ya fedha yake na dhahabu na kwa ajili ya vito vyake vya thamani, vikolezi, ngao na aina zote za vyombo vya thamani. Akajenga pia maghala ya kuhifadhi mavuno ya nafaka, divai mpya na mafuta. Akatengeneza mabanda kwa ajili ya aina mbalimbali za mifugo, na mazizi kwa ajili ya kondoo na mbuzi. Akajenga vijiji na kujipatia idadi kubwa ya kondoo na mbuzi, pamoja na ngʼombe kwa kuwa Mungu alikuwa amempa utajiri mwingi sana. Ilikuwa ni Hezekia aliyeziba njia za kutolea maji za chemchemi za juu za Gihoni na kuyaelekeza maji kutiririkia upande wa magharibi wa Mji wa Daudi. Akafanikiwa katika kila kitu alichofanya. (2 Nyakati 32:27-30)
Wakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi. (Nehemia 9:25)
...naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu mkuu sana miongoni mwa watu wa Mashariki. (Ayubu 1:3)
Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli. (Danieli 3:30)
Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. (Mathayo 27:57)
Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi! Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, (1 Wakorintho 4:8, 11-12)
Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. (Wafilipi 4:11-18)

Bwana hufurahia kufanikiwa kwa watumishi wake

Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.” (Zaburi 35:27)

Si wote watakaofanikiwa

Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini. Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi. (Waebrania 11:36-40)

Yesu anastahili kupokea utajiri

Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!” (Ufunuo 5:12)

Wenye hekima wanaweza kutajirika

Utajiri wa wenye hekima ni taji yao, bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu. (Mithali 14:24)

Jinsi utajiri unavyopatikana

Kwa hekima nyumba hujengwa, nayo kwa njia ya ufahamu huimarishwa kwa njia ya maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza. (Mithali 24:3-4)

Mambo yanayowazuia watu kupata utajiri

Mtu apendaye anasa atakuwa maskini, yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri. (Mithali 21:17)
Yeye amwoneaye maskini ili kujiongezea mali, naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini. (Mithali 22:16)

Hatari za utajiri

Kupenda utajiri

Usitumainie vya udhalimu wala usijivune kwa vitu vya wizi; ingawa utajiri wako utaongezeka, usiviwekee moyo wako. (Zaburi 62:10)

Kiburi

Kwa hekima yako na ufahamu wako, umejipatia utajiri, nawe umejikusanyia dhahabu na fedha katika hazina zako. Kwa werevu wako mwingi katika biashara, umeongeza utajiri wako na kwa sababu ya utajiri wako moyo wako umekuwa na kiburi. (Ezekieli 28:4-5)
Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. (1 Timotheo 6:17)

Matajiri hawapaswi kujivuna kwa sababu maisha ni mafupi

Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. Kwa maana jua kali lenye kuchoma huchomoza na kuliunguza, likayakausha majani, na ua lake likapukutika, nao uzuri wake huharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake. (Yakobo 1:9-11)

Jivunie Bwana, si utajiri

Hili ndilo asemalo Bwana: “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake, au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake, wala tajiri ajisifu katika utajiri wake, lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili: kwamba ananifahamu na kunijua mimi, kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema, hukumu na haki duniani, kwa kuwa napendezwa na haya,” asema Bwana. (Yeremia 9:23-24)

Utajiri hutoa hisia ya usalama

Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, bali ufukara ni maangamizi ya maskini. (Mithali 10:15)
Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa. (Mithali 18:11)
Nilipofanikiwa nilisema, “Sitatikiswa kamwe.” Ee Bwana, uliponijalia, uliuimarisha mlima wangu, lakini ulipouficha uso wako nilifadhaika. (Zaburi 30:6-7)

Wale wanaotumainia utajiri

Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa; wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia na kuwaachia wengine mali zao. Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele, makao yao vizazi vyote; ingawa walikuwa na mashamba na kuyaita kwa majina yao. Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu; anafanana na mnyama aangamiaye. (Zaburi 49:10-12)

Utajiri huelekea kuwatenganisha watu

Basi Loti, ambaye alikuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na makundi ya mbuzi, kondoo, ngʼombe na mahema. Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali zao. Ukazuka ugomvi kati ya wachunga mifugo wa Abramu na wale wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Hivyo Abramu akamwambia Loti, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Kama ukielekea kushoto, nitakwenda kulia; kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.” Loti akatazama akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora.) Hivyo Loti akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana: (Mwanzo 13:5-11)
Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaki, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” (Mwanzo 26:12-16)
Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike na wote wa nyumbani mwake, mifugo yake pamoja na wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata akiwa Kanaani, akahamia katika nchi iliyo mbali na Yakobo ndugu yake. Mali zao zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba haikuwa rahisi wao kuishi pamoja, nchi waliyokuwa wakiishi isingewatosha wote kwa ajili ya mifugo yao. (Mwanzo 36:6-7)
Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi. (Isaya 5:8)

Utajiri unaweza kuwatenganisha Wakristo

Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha! (1 Wakorintho 11:18-22)

Utajiri ni wa udanganyifu/unaweza kusonga kuzaa matunda

Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu, bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika. (Mithali 11:18)
Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. (Mathayo 13:4-5, 7, 22)
Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema: “Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao. Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno; lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae. (Marko 4:2-3, 7, 18-19)
Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea. Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. (Luka 8:7, 14)

Ni vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme

Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.” Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.” Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?” Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.” (Mathayo 19:16-26)
Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ” Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.” Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika Ufalme wa Mungu!” Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika Ufalme wa Mungu. Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.” (Marko 10:17-27)
Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!” Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.” (Luka 18:28-30)

Matajiri wasiomjua Bwana watatengwa naye milele

“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake. “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’ “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. (Luka 16:19-25)

Matajiri hudhani wana hekima

Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua. (Mithali 28:11)

Jinsi matajiri wanavyowatendea maskini

Mtu maskini huomba kuhurumiwa bali tajiri hujibu kwa ukali. (Mithali 18:23)
Matajiri huwatawala maskini naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye. (Mithali 22:7)
Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa? (Yakobo 2:6-7)

Utajiri unaweza kuchangia kumsahau Bwana

Wakati Bwana Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaki na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, ina miji inayopendeza ambayo hukuijenga, nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba, jihadhari usije ukamwacha Bwana, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. (Kumbukumbu 6:10-12)
...nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kutoka kwenye vilima. Wakati mtakapokwisha kula na kushiba, msifuni Bwana Mungu wenu kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa. Jihadharini msimsahau Bwana Mungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo. Angalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo, na wakati makundi yenu ya ngʼombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa, basi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahau Bwana Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. Aliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu. Aliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekesha na kuwajaribu ninyi ili mwishoni apate kuwatendea mema. Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo. (Kumbukumbu 8:9-18)
Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja Agano langu. (Kumbukumbu 31:20)
“Ninakuomba vitu viwili, Ee Bwana; usininyime kabla sijafa: Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo; usinipe umaskini wala utajiri, bali unipe chakula cha kunitosha kila siku. Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana na kusema, ‘Bwana ni nani?’ Au nisije nikawa maskini nikaiba, nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu. (Mithali 30:7-9)
Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama, lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’ Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako; hujanitii mimi. Upepo utawaondoa wachungaji wako wote, na wale ulioungana nao wataenda uhamishoni. Kisha utaaibika na kufedheheka kwa sababu ya uovu wako wote. (Yeremia 22:21-22)
Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona. (Ufunuo 3:17-18)

Utajiri huleta wivu

Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. (Mwanzo 26:12-14)
Ndipo Abimeleki akamwambia Isaki, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” (Mwanzo 26:16)
Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua kila kitu kilichokuwa cha baba yetu naye amepata utajiri huu wote kutokana na vile vilivyokuwa mali ya baba yetu.” (Mwanzo 31:1)

Laana za utajiri

Laana ya kutekwa nyara

Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho. (Mithali 13:8)

Laana ya kukosa usingizi

Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe amekula kidogo au kingi, lakini wingi wa mali humnyima tajiri usingizi. (Mhubiri 5:12)

Ole uliotamkwa juu ya matajiri

“Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu. (Luka 6:24)
Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote. Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. (Yakobo 5:1-5)

Kwa nini waovu hufanikiwa?

Hujivunia tamaa za moyo wake; humbariki mlafi na kumtukana Bwana. Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu, katika mawazo yake yote hakuna nafasi ya Mungu. Njia zake daima hufanikiwa; hujivuna na amri zako ziko mbali naye, huwacheka kwa dharau adui zake wote. (Zaburi 10:3-5)
Zaburi ya Daudi. Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya, kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara. Tulia mbele za Bwana na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu. Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi. Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana. Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele. (Zaburi 37:1-2, 7, 9-11)
Zaburi ya Asafu. Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa wale ambao mioyo yao ni safi. Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza; nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama. Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna nilipoona kufanikiwa kwa waovu. Wao hawana taabu, miili yao ina afya na nguvu. Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine, wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine. Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao, wamejivika jeuri. Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi, majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo. Hudhihaki na kusema kwa ukorofi, katika majivuno yao wanatishia kutesa. Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu, nazo ndimi zao humiliki duniani. Kwa hiyo watu wao huwageukia na kunywa maji tele. Wanasema, “Mungu awezaje kujua? Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?” Hivi ndivyo walivyo waovu: siku zote hawajali, wanaongezeka katika utajiri. Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia. Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi. Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningelikuwa nimewasaliti watoto wako. Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa. Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilipotambua mwisho wao. Hakika unawaweka mahali pa utelezi, unawaangusha chini kwa uharibifu. Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula, wanatoweshwa kabisa na vitisho! Kama ndoto mtu aamkapo, hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana, utawatowesha kama ndoto. (Zaburi 73:1-20)
Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima, bali wanaume wakorofi hupata mali tu. (Mithali 11:16)
Wewe daima u mwenye haki, Ee Bwana, niletapo mashtaka mbele yako. Hata hivyo nitazungumza nawe kuhusu hukumu yako: Kwa nini njia ya waovu inafanikiwa? Kwa nini wasio waaminifu wote wanaishi kwa raha? Umewapanda, nao wameota, wanakua na kuzaa matunda. Daima u midomoni mwao, lakini mbali na mioyo yao. (Yeremia 12:1-2)

Matajiri wasiomcha Mungu

Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli. (1 Samweli 25:2)
Kwa siku zote 180 mfalme alionyesha utajiri mwingi wa ufalme wake, fahari na utukufu wa enzi yake. (Esta 1:4)
Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine. (Esta 5:11)
Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hakuna mwisho wa hazina zao. Nchi yao imejaa farasi, hakuna mwisho wa magari yao. (Isaya 2:7)
Wakati bidhaa zako zilipotoka baharini, ulitosheleza mataifa mengi; kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako ulitajirisha wafalme wa dunia. (Ezekieli 27:33)
“Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme watatu zaidi watatokea Uajemi, kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Wakati atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani. (Danieli 11:2)
Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo. (Luka 19:2)

Amri ya kutotafuta kufanikiwa kwa watu fulani

Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote. (Kumbukumbu 23:6)
Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’ (Ezra 9:12)

Njia mbaya ya kufanikiwa

Wengine hufanikiwa kwa kutenda dhambi bila kukiri dhambi yao

Efraimu hujisifu akisema, “Mimi ni tajiri sana; nimetajirika. Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu uovu wowote au dhambi.” (Hosea 12:8)
Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘Bwana asifiwe, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii. (Zekaria 11:5)

Wengine hujifanya wa kidini ili wafanikiwe

Ndipo Mika akasema, “Sasa najua Bwana atanitendea mema, kwa kuwa Mlawi huyu amekuwa kuhani wangu.” (Waamuzi 17:13)

Mengineyo

...na kama utaitafuta kama fedha na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa, (Mithali 2:4)
Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako, au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala, kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako, naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema. (Mhubiri 10:20)

Watu wakati mwingine hudanganya kuhusu hali yao ya kifedha

Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi. (Mithali 13:7)

Fedha zimetumika kuonyesha thamani ya Ufalme wa Mungu

“Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.” “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.” (Mathayo 13:44-46)

Maisha ya haki yanalinganishwa na fedha safi

Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora, bali moyo wa mwovu una thamani ndogo. (Mithali 10:20)

Hukumu juu ya mataifa tajiri yasiyomcha Mungu

Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi. (Isaya 15:7)
Wewe uishiye kando ya maji mengi na uliye na wingi wa hazina, mwisho wako umekuja, wakati wako wa kukatiliwa mbali. (Yeremia 51:13)
Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “ ‘Ee Tiro, wewe umesema, “Mimi ni mkamilifu katika uzuri.” “ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali zako. “ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, walibadilisha watumwa na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako. “ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali zako. “ ‘Watu wa Dedani walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo. “ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe na akiki nyekundu. “ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe, walibadilishana kwa ngano kutoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri ya kuponyeshea. “ ‘Dameski, kwa sababu ya wingi wa kazi za mikono yako na ukuu wa utajiri wa mali, walifanya biashara nawe wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari. “ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali, walikuletea mali za biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai. “ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi. “ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako waliobadilishana bidhaa zako na wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi. “ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezi, vito vya thamani na dhahabu. “ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara. “ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo zinazokusafirishia bidhaa zako. Umejazwa shehena kubwa katika moyo wa bahari. Wapiga makasia wako wanakupeleka mpaka kwenye maji makavu. Lakini upepo wa mashariki umekuvunja vipande vipande katika moyo wa bahari. Utajiri wako, bidhaa zako na mali zako, mabaharia wako, manahodha wako, mafundi wako wa meli, wafanyabiashara wako na askari wako wote, na kila mmoja aliyeko melini atazama kwenye moyo wa bahari siku ile ya kuvunjika kwa meli yako. (Ezekieli 27:3, 12-27)
Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana, alijizalia matunda mwenyewe. Kadiri matunda yake yalivyoongezeka, alijenga madhabahu zaidi; kadiri nchi yake ilivyostawi, alipamba mawe yake ya ibada. Moyo wao ni mdanganyifu, nao sasa lazima wachukue hatia yao. Bwana atabomoa madhabahu zao na kuharibu mawe yao ya ibada. (Hosea 10:1-2)
Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni; wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa, wote ambao wanafanya biashara ya fedha wataangamizwa. Utajiri wao utatekwa nyara, nyumba zao zitabomolewa. Watajenga nyumba, lakini hawataishi ndani yake; watapanda mizabibu lakini hawatakunywa divai yake. Fedha yao wala dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana. Katika moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa, kwa maana ataleta mwisho wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.” (Sefania 1:11, 13, 18)
Tiro amejijengea ngome imara, amelundika fedha kama mavumbi na dhahabu kama taka za mitaani. Lakini Bwana atamwondolea mali zake na kuuangamiza uwezo wake wa baharini, naye atateketezwa kwa moto. (Zekaria 9:3-4)

Mfalme hakupaswa kutajirika kupita kiasi

Hata hivyo, kamwe mfalme asijipatie hesabu kubwa ya farasi kwa ajili yake mwenyewe, au kuwafanya watu warudi Misri ili kupata farasi zaidi, kwa maana Bwana amekuambia, “Hamtairudia njia ile tena.” Kamwe asioe wake wengi, la sivyo moyo wake utapotoka. Kamwe asijilimbikizie kiasi kikubwa cha fedha na dhahabu. (Kumbukumbu 17:16-17)

Wafalme hawakutii amri ya kutotajirika kupita kiasi

Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 ya magari ya vita, na farasi 12,000. (1 Wafalme 4:26)
Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666, mbali na mapato kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Kiarabu na watawala wa nchi. Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni. Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na egemeo la nyuma lilikuwa la mviringo kwa juu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote. Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo siku za Solomoni. Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo. Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake. Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu. Solomoni akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000, ambayo aliyaweka katika miji ya magari na mengine akawa nayo huko Yerusalemu. Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani. Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue. (1 Wafalme 10:14-28)
Solomoni akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000, ambayo aliyaweka katika miji ya magari na mengine akawa nayo huko Yerusalemu. Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa vitu vya kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani. Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue. Waliagiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha, na farasi kwa shekeli 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu. (2 Nyakati 1:14-17)
Ahimidiwe Bwana Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe, na akakuweka juu ya kiti chake cha ufalme utawale kwa niaba ya Bwana Mungu wako. Kwa sababu ya upendo wa Mungu wako kwa Israeli na shauku yake ya kuwadhibitisha milele, amekufanya wewe mfalme juu yao, ili kudumisha haki na uadilifu.” Naye akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa vikolezi vizuri kama vile Malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni. (Watumishi wa Hiramu na wa Solomoni wakaleta dhahabu kutoka Ofiri, tena wakaleta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani. Mfalme akatumia hiyo miti ya msandali kuwa ngazi kwa ajili ya Hekalu la Bwana na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa Yuda tangu siku ile.) Mfalme Solomoni akampa Malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, zaidi ya vile alivyokuwa amemletea mfalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake. Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666, mbali na mapato yaliyoletwa na wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Solomoni dhahabu na fedha. Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni. Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pa kuwekea miguu vyote vya dhahabu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote. Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Solomoni. Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizoendeshwa na watu wa Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo. Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. Wafalme wote wa dunia wakatafuta kukutana na Solomoni ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake. Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu. Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 kwa ajili ya farasi na magari ya vita, farasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita na katika Yerusalemu pamoja naye. Solomoni akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto Frati mpaka kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri. Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani. (2 Nyakati 9:8-27)

Unabii

Binti wa Tiro atakuletea zawadi, watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako. (Zaburi 45:12)
Hezekia akawapokea wale wajumbe kwa furaha na kuwaonyesha vitu vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha lote, na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha. Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?” Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.” Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote: Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. (Isaya 39:2, 4-6)
Ndipo utatazama na kutiwa nuru, moyo wako utasisimka na kujaa furaha, mali zilizo baharini zitaletwa kwako, utajiri wa mataifa utakujilia. Makundi ya ngamia yatajaa katika nchi yako, ngamia vijana wa Midiani na Efa. Nao wote watokao Sheba watakuja, wakichukua dhahabu na uvumba na kutangaza sifa za Bwana. Hakika visiwa vinanitazama, merikebu za Tarshishi ndizo zinazotangulia, zikiwaleta wana wenu kutoka mbali, wakiwa na fedha na dhahabu zao, kwa heshima ya Bwana, Mungu wenu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekujalia utukufu. Malango yako yatakuwa wazi siku zote, kamwe hayatafungwa, mchana wala usiku, ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa: wafalme wao wakiongoza maandamano ya ushindi. (Isaya 60:5-6, 9, 11)
Nanyi mtaitwa makuhani wa Bwana, mtaitwa watumishi wa Mungu wetu. Mtakula utajiri wa mataifa, nanyi katika utajiri wao mtajisifu. Badala ya aibu yao watu wangu watapokea sehemu maradufu, na badala ya fedheha watafurahia katika urithi wao; hivyo watarithi sehemu maradufu katika nchi yao, nayo furaha ya milele itakuwa yao. (Isaya 61:6-7)
Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. (Hagai 2:7)
“Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Bwana atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ” (Zekaria 1:17)
Je, haya sio maneno ya Bwana aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefala zikiwa zimekaliwa na watu?’ ” (Zekaria 7:7)
Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! (Ufunuo 6:15-16)
Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye kipaji chake cha uso, ili kwamba mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake. (Ufunuo 13:16-17)
Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake. (Ufunuo 17:4)
Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao, nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.” (Ufunuo 18:3)
“Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena: Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marmar, bidhaa za mdalasini, vikolezi, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ngʼombe na kondoo; farasi na magari; na miili na roho za wanadamu. “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’ Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi, ya rangi ya zambarau na nyekundu, ukimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu! Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa kama huu umeangamia!’ “Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali. Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, mji ambao wote wenye meli baharini walitajirika kupitia kwa mali zake! Katika saa moja tu ameangamizwa! (Ufunuo 18:11-19)

Matarajio ya utajiri yametumika kama motisha

Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.” Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Na nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema. Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.” (Mwanzo 34:10-12)
Wakasema, “Hawa watu ni marafiki kwetu, tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake, nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao. Nao wanaweza kuoa binti zetu. Je, si mifugo yao, mali zao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi na tuwape kibali, nao wataishi miongoni mwetu.” (Mwanzo 34:21, 23)
Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.” (1 Samweli 17:25)