Watu si waaminifu
Moyo wa mwanadamu si mwaminifu
Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya. (Mwanzo 8:21)
Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote, ni mwovu kupita kiasi. Ni nani awezaye kuujua? (Yeremia 17:9)
Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. (Mathayo 15:19)
Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. (Marko 7:21-22)
Watu hufanya uaminifu wa kiasi
Katika siku hizo Israeli hawakuwa na mfalme, kila mmoja akafanya kama alivyoona vyema machoni pake mwenyewe. (Waamuzi 17:6)
Mifano ya watu wasio waaminifu
...hata hivyo baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru. (Mwanzo 31:7)
Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao. Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya: Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.” (Yoshua 7:11, 20-21)
Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki. (1 Samweli 8:3)
Umwambie, ‘Hivi ndivyo Bwana asemavyo: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Mahali ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako, naam, yako wewe!’ ” (1 Wafalme 21:19)
Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao, toka tumboni mwa mama zao ni wakaidi na husema uongo. (Zaburi 58:3)
Watawala wenu ni waasi, rafiki wa wevi, wote wanapenda rushwa na kukimbilia hongo. Hawatetei yatima, shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe. (Isaya 1:23)
Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe. (Isaya 56:11)
“Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata faida zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. (Yeremia 6:13)
“ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyangʼanyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! asema Bwana. (Yeremia 7:9, 11)
Maafisa wake walioko ndani yake ni kama mbwa mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu. Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki. (Ezekieli 22:27, 29)
Sikieni neno la Bwana, enyi Waisraeli, kwa sababu Bwana analo shtaka dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi: “Hakuna uaminifu, hakuna upendo, hakuna kumjua Mungu katika nchi. Kuna kulaani tu, uongo na uuaji, wizi na uzinzi, bila kuwa na mipaka, nao umwagaji damu mmoja baada ya mwingine. (Hosea 4:1-2)
Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji. (Hosea 5:10)
...kila mara nilipotaka kumponya Israeli, dhambi za Efraimu zinafichuliwa na maovu ya Samaria yanafunuliwa. Wanafanya udanganyifu, wevi huvunja nyumba, maharamia hunyangʼanya barabarani, (Hosea 7:1)
Mfanyabiashara hutumia vipimo vya udanganyifu; hupenda kupunja. (Hosea 12:7)
Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu, hazina yako uliyopata kwa udanganyifu na vipimo vilivyopunguka, ambavyo vimelaaniwa? Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo? Matajiri wake ni wajeuri; watu wake ni waongo na ndimi zao zinazungumza kwa udanganyifu. (Mika 6:10-12)
Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye angemsaliti Yesu, akasema, “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300 na fedha hizo wakapewa maskini?” Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi, kwani ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo. (Yohana 12:4-6)
Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyangʼanyi. (Yohana 18:40)
Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume. Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.” Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika. Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.” Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.” Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. (Matendo 5:1-10)
Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.” (Tito 1:12)
Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea. Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao. (Ufunuo 9:20-21)
Mfano unaotumia udanganyifu kama kielelezo
Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Ilisemekana kwamba huyo msimamizi alikuwa anatumia vibaya mali ya tajiri yake. Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’ “Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba. Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani kwao.’ “Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’ “Akajibu, ‘Galoni 800 za mafuta ya mizeituni.’ “Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400.’ “Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’ “Akajibu, ‘Vipimo 1,000 vya ngano.’ “Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, andika vipimo 800!’ “Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru. (Luka 16:1-8)
Udanganyifu uliofichwa ndani ya dini
“ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza? Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyangʼanyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! asema Bwana. (Yeremia 7:9-11)
Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.” (Mathayo 21:12-13)
“Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na kutokuwa na kiasi. (Mathayo 23:25)
Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” (Marko 11:15-17)
Ndipo Bwana akamwambia, “Sasa, enyi Mafarisayo, mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na uovu. (Luka 11:39)
Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo. Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” (Luka 19:45-46)
Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu. (Tito 1:10-11)
Mungu anadai uaminifu kamili
Bwana ni kweli, Shetani ni mwongo
Bwana ni kweli
Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. (Yohana 1:14)
Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. (Yohana 14:6)
Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. (Yohana 16:13)
Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho Mtakatifu. Hawa watatu ni umoja. (1 Yohana 5:7)
Shetani ni mwongo
Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. (Yohana 8:44)
Chini ya sheria ya Agano la Kale
Usiibe. (Kutoka 20:15)
“ ‘Usiibe. “ ‘Usiseme uongo. “ ‘Msidanganyane. “ ‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana. “ ‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako. “ ‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi. (Walawi 19:11-13)
“ ‘Usitumie vipimo vya udanganyifu unapopima urefu, kupima uzito, wala kupima wingi. Tumia mizani halali, mawe ya kupimia uzito halali, efa halali, na hini halali. Mimi ndimi Bwana Mungu wako, ambaye alikutoa katika nchi ya Misri. (Walawi 19:35-36)
“ ‘Ikiwa utauza ardhi kwa mmoja wa wazawa wa nchi yako, au ukinunua ardhi kutoka kwake, mmoja asimpunje mwingine. Utanunua ardhi kwa mzawa wa nchi yako kwa misingi ya hesabu ya miaka baada ya Yubile. Naye ataiuza kwako kwa misingi ya hesabu ya miaka iliyobaki kwa kuvuna mavuno. Miaka inapokuwa mingi, utaongeza bei, nayo miaka ikiwa michache, utapunguza bei, kwa sababu kile anachokuuzia kwa hakika ni hesabu ya mazao. Mmoja asimpunje mwingine, bali utamcha Mungu wako. Mimi ndimi Bwana Mungu wako. (Walawi 25:14-17)
Usiibe. (Kumbukumbu 5:19)
Usisogeze jiwe la mpaka wa jirani yako ambao uliwekwa na wale waliokutangulia katika urithi upokeao katika nchi Bwana Mungu wako anayowapa kuimiliki. (Kumbukumbu 19:14)
Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako. Kwa maana Bwana Mungu wako humchukia yeyote ambaye hufanya mambo kama haya, yeyote anayetenda kwa udanganyifu. (Kumbukumbu 25:13-16)
Kama kanuni ya jumla ya Biblia
...basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo. (Zaburi 34:13)
Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima. (Zaburi 51:6)
Usitumainie vya udhalimu wala usijivune kwa vitu vya wizi; ingawa utajiri wako utaongezeka, usiviwekee moyo wako. (Zaburi 62:10)
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako. (Mithali 3:3)
Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako. (Mithali 4:24)
Mtu mbaya sana na mlaghai, ambaye huzungukazunguka na maneno ya upotovu, (Mithali 6:12)
Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake: shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo, na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu. (Mithali 6:16, 19)
Bwana huchukia sana mizani za udanganyifu, bali vipimo sahihi ni furaha yake. (Mithali 11:1)
Bwana anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli. (Mithali 12:22)
Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha. (Mithali 13:5)
Shahidi mwaminifu hadanganyi, bali shahidi wa uongo humimina uongo. (Mithali 14:5)
Shahidi wa kweli huokoa maisha, bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu. (Mithali 14:25)
Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu: je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala! (Mithali 17:7)
Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Bwana; mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye. (Mithali 16:11)
Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, Bwana huchukia vyote viwili. (Mithali 20:10)
Bwana anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi. (Mithali 20:23)
Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini, wala kumdhulumu mhitaji mahakamani, kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao naye atawateka wao waliowateka. (Mithali 22:22-23)
Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani lililowekwa na baba zako. (Mithali 22:28)
Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima, (Mithali 23:10)
Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu. (Mithali 23:23)
Yeye amwibiaye babaye au mamaye na kusema, “Si kosa,” yeye ni mwenzi wa yule aharibuye. (Mithali 28:24)
Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana, kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya? (Maombolezo 3:35-36)
Haya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia yote haya,” asema Bwana. (Zekaria 8:16-17)
Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?” Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.” Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?” Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.” (Luka 3:12-14)
...basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? (Warumi 2:21-22)
Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa? Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu. Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. (1 Wakorintho 6:7-10)
Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. (Waefeso 4:25)
Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, (Waefeso 6:14)
Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, (Wakolosai 3:9)
Jiepusheni na uovu wa kila namna. (1 Wathesalonike 5:22)
Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji, kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli, (1 Timotheo 1:9-10)
Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao, wala wasiwaibie, bali waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu yawe ya kuvutia. (Tito 2:9-10)
Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” (1 Petro 1:15-16)
Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine. (1 Petro 4:15)
Inatakiwa kwa viongozi
Serikali
Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. (Kutoka 18:21-22)
Upendo na uaminifu humweka mfalme salama, kwa njia ya upendo, kiti chake cha enzi huwa salama. (Mithali 20:28)
Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu. (Mithali 28:16)
“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asema Bwana Mwenyezi. Tumieni mizani sahihi na vipimo sahihi vya efa na bathi. (Ezekieli 45:9-10)
Kanisa
Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. (1 Timotheo 3:8)
Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. (Tito 1:7)
Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. (1 Petro 5:1-2)
Uaminifu unatakiwa katika kutoa
Nanyi mnasema, ‘Mzigo gani huu!’ Nanyi mnaidharau kwa kiburi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Wakati mnapowaleta wanyama mliopokonya kwa nguvu, walio vilema au walio wagonjwa na kuwatoa kama dhabihu, je, niwakubali kutoka mikononi mwenu?” asema Bwana. “Amelaaniwa yeye adanganyaye, aliye na mnyama wa kiume anayekubalika katika kundi lake na kuweka nadhiri ya kumtoa, lakini akatoa dhabihu ya mnyama aliye na dosari kwa Bwana. Kwa kuwa mimi ni Mfalme Mkuu, nalo Jina langu linapaswa kuogopwa miongoni mwa mataifa,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. (Malaki 1:13-14)
Kutotoa ipasavyo kunaonekana kama wizi
“Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi. “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’ “Mnaniibia zaka na dhabihu. Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. (Malaki 3:8-9)
Uaminifu una thamani kuliko mali
Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka. (Mithali 19:1)
Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo. (Mithali 19:22)
Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa, bali waovu watawalapo, watu hujificha. (Mithali 28:12)
Mifano ya watu waaminifu
Ndipo Mose akakasirika sana na kumwambia Bwana, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua chochote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.” (Hesabu 16:15)
Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni juu yangu mbele za Bwana na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Ni nani nimepata kumwonea? Ni kutoka kwenye mkono wa nani nimepokea rushwa ili kunifanya nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, mimi nitawarudishia.” Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutuonea. Hujapokea chochote kutoka kwenye mkono wa mtu awaye yote.” Samweli akawaambia, “Bwana ni shahidi juu yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.” Wakasema, “Yeye ni shahidi.” (1 Samweli 12:3-5)
“Kama nimeishi katika uongo au mguu wangu umekimbilia udanganyifu, basi wengine na wale nilichokipanda, nayo yale yote niliyootesha na yangʼolewe. (Ayubu 31:5, 8)
Walipofahamu hilo, wakuu na wasimamizi wakajaribu kutafuta sababu za kumshtaki Danieli kuhusu usimamizi wake wa shughuli za serikali, lakini hawakuweza kufanikiwa. Hawakuweza kupata kosa kwake, kwa sababu alikuwa mwaminifu, wala hakupatikana na upotovu au uzembe. (Danieli 6:4)
Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lolote baya mbele yako, ee mfalme.” (Danieli 6:22)
Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa; hawatasema uongo, wala udanganyifu hautakuwa katika vinywa vyao. Watakula na kulala wala hakuna yeyote atakayewaogopesha.” (Sefania 3:13)
Mfano wa kupima uaminifu wa watu
Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.” Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu: Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa. Lakini ni lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo. (Mwanzo 42:11, 18-20)
Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi. Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’ “Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa. Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ” (Mwanzo 42:31-34)
Wanaomcha Mungu huchukia udanganyifu
Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha. (Mithali 13:5)
Kwa nini Mungu anadai uaminifu kamili?
Hatuwezi kuwa wadanganyifu na kumpenda Mungu
Yeye ambaye njia zake ni nyofu humcha Bwana, bali yeye ambaye njia zake zimepotoka humdharau Mungu. (Mithali 14:2)
Hatuwezi kuwa wadanganyifu na kumpenda jirani yetu
Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza, nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu. (Mithali 26:28)
Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa sheria. (Warumi 13:9-10)
Uaminifu hufanya uinjilisti uaminike
...ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. (Wafilipi 2:15)
Uaminifu husaidia kuongoza maisha yetu
Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako. Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako. Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika. (Mithali 4:24-26)
Hata udanganyifu mdogo kabisa huharibu
“Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. (Luka 16:10)
Tunawezaje kuepuka jaribu la kutokuwa waaminifu?
Kwa neema na uwezo wa Bwana
Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi. (Zaburi 119:36)
“Ninakuomba vitu viwili, Ee Bwana; usininyime kabla sijafa: Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo; usinipe umaskini wala utajiri, bali unipe chakula cha kunitosha kila siku. (Mithali 30:7-8)
Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. (Wagalatia 5:16-17)
Kwa kutenda kanuni ya dhahabu
Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii. (Mathayo 7:12)
Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine. (Wafilipi 2:4)
Kwa kumcha Bwana ipasavyo
Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa; kwa kumcha Bwana mtu hujiepusha na ubaya. (Mithali 16:6)
Kujitenga na wadanganyifu
Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki, (Zaburi 26:4)
Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake, asiyewategemea wenye kiburi, wale wenye kugeukia miungu ya uongo. (Zaburi 40:4)
Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, ili waweze kuishi pamoja nami; yeye ambaye moyo wake hauna lawama atanitumikia. Mdanganyifu hatakaa nyumbani mwangu, yeye asemaye kwa uongo hatasimama mbele yangu. (Zaburi 101:6-7)
Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi, usikubaliane nao. Kama wakisema, “Twende tufuatane; tukamvizie mtu na kumwaga damu, njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia; tuwameze wakiwa hai kama kaburi, wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni. Tutapata aina zote za vitu vya thamani na kujaza nyumba zetu kwa nyara. Njoo ushirikiane nasi, vitu vyote tutakavyopata tutagawana.” Mwanangu, usiandamane nao. Usiweke mguu wako katika njia zao, kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni wepesi kumwaga damu. (Mithali 1:10-16)
Anayekubaliana na mwizi ni adui wa nafsi yake mwenyewe; huapishwa lakini hathubutu kushuhudia. (Mithali 29:24)
Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi. Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyangʼanyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu. Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye. (1 Wakorintho 5:9-11)
Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” (1 Wakorintho 15:33)
Kwa kutoa
Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji. (Waefeso 4:28)
Kwa kuweka mfumo wa uwajibikaji
Labani akamuuliza, “Nikupe nini?” Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako. Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabakabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabakabaka. Hawa watakuwa ujira wangu. Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabakabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.” (Mwanzo 30:31-33)
Tufanye nini tunapokuwa tumetenda udanganyifu?
Kurejesha ushirika wetu na Bwana
“ ‘Wakati mtu yeyote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, lazima akiri ni kwa njia gani ametenda dhambi, na kama adhabu ya dhambi aliyoitenda, lazima alete kwa Bwana kondoo jike au mbuzi jike kutoka kwenye kundi lake kama sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yake. (Walawi 5:5-6)
Bwana akamwambia Mose: “Kama mtu yeyote akitenda dhambi, naye si mwaminifu kwa Bwana kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa, au kimeachwa chini ya utunzaji wake, au kimeibwa, au kama akimdanganya, au akiokota mali iliyopotea na akadanganya, au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yoyote ambayo watu waweza kuitenda; wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata, au chochote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, na aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, vyote ampe mwenye mali siku ile anapeleka sadaka yake ya hatia. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa kwa kosa lolote katika mambo hayo aliyoyatenda yaliyomfanya kuwa na hatia.” (Walawi 6:1-5, 7)
Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. (1 Yohana 1:9)
Kurejesha uhusiano wetu na mtu tuliyemdhuru
Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema. (Mithali 28:13)
Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana. (Yakobo 5:16)
Kurudisha chochote kilichoibwa
“Kama mtu akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ngʼombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. “Kama mwizi akishikwa anavunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu; lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu. “Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake. “Kama mnyama aliyeibwa akikutwa hai mikononi mwake, ikiwa ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili. (Kutoka 22:1-4)
“Kama mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, na kama vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi atashikwa, lazima alipe mara mbili. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake. Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, ikiwa ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea ambayo fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ pande zote mbili wataleta mashauri yao mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watamwona kuwa na hatia atamlipa jirani yake mara mbili. (Kutoka 22:7-9)
“Kama mtu akimwazima mnyama kutoka kwa jirani yake, na kama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama. (Kutoka 22:14)
Bwana akamwambia Mose: “Kama mtu yeyote akitenda dhambi, naye si mwaminifu kwa Bwana kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa, au kimeachwa chini ya utunzaji wake, au kimeibwa, au kama akimdanganya, au akiokota mali iliyopotea na akadanganya, au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yoyote ambayo watu waweza kuitenda; wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata, au chochote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, na aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, vyote ampe mwenye mali siku ile anapeleka sadaka yake ya hatia. (Walawi 6:1-5)
Bwana akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Wakati mwanaume au mwanamke akimkosea mwenzake kwa njia yoyote, na kwa hivyo akawa si mwaminifu kwa Bwana, mtu huyo ana hatia, na ni lazima atubu dhambi aliyoifanya. Ni lazima atoe malipo kamili kwa ajili ya kosa lake, aongeze sehemu ya tano juu ya malipo hayo na kutoa yote kwa mtu aliyemkosea. Lakini ikiwa mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye malipo yanaweza kufanywa kwa ajili ya kosa, malipo yatakuwa mali ya Bwana, nayo ni lazima apewe kuhani, pamoja na kondoo dume ambaye anatumika kufanyia upatanisho kwa ajili yake. (Hesabu 5:5-8)
Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Bwana aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.” (2 Samweli 12:5-6)
Watu hawamdharau mwizi kama akiiba kukidhi njaa yake wakati ana njaa. Pamoja na hayo, kama akikamatwa, lazima alipe mara saba, ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake. (Mithali 6:30-31)
Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi. (Ezekieli 33:14-16)
Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.” (Luka 19:8)
Baraka na laana
Baraka zilizoahidiwa kwa waaminifu
Baraka ya uhusiano wa karibu zaidi na Bwana
Zaburi ya Daudi. Bwana, ni nani awezaye kukaa katika Hekalu lako? Nani awezaye kuishi katika mlima wako mtakatifu? Ni yule aendaye pasipo mawaa, atendaye yaliyo haki, asemaye kweli toka moyoni mwake, na hana masingizio ulimini mwake, asiyemtenda jirani yake vibaya, na asiyemsingizia mwenzake, ambaye humdharau mtu mbaya, lakini huwaheshimu wale wamwogopao Bwana, yule atunzaye kiapo chake hata kama anaumia. (Zaburi 15:1-4)
Nani awezaye kuupanda mlima wa Bwana? Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake? Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe, yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake au kuapa kwa kitu cha uongo. (Zaburi 24:3-4)
Bwana yu karibu na wote wamwitao, karibu na wote wamwitao kwa uaminifu. (Zaburi 145:18)
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako. Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu. (Mithali 3:3-4)
...kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu, lakini siri yake iko kwa mwenye haki. (Mithali 3:32)
Bwana anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli. (Mithali 12:22)
“Je, inakufanya kuwa mfalme huko kuongeza idadi ya mierezi? Je, baba yako hakuwa na chakula na kinywaji? Alifanya yaliyo sawa na haki, hivyo yeye akafanikiwa katika yote. Aliwatetea maskini na wahitaji, hivyo yeye akafanikiwa katika yote. Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?” asema Bwana. “Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu katika mapato ya udhalimu, kwa kumwaga damu isiyo na hatia, kwa uonevu na ukatili.” (Yeremia 22:15-17)
Baraka ya ulinzi
Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu, yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama, (Mithali 2:7)
Mtu mwadilifu hutembea salama, lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa. (Mithali 10:9)
Baraka ya riziki
Yeye aendaye kwa uadilifu na kusema lililo haki, yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma na kuizuia mikono yake isipokee rushwa, yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji, na yeye afumbaye macho yake yasitazame sana uovu: huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu, ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani. Atapewa mkate wake, na maji yake hayatakoma. (Isaya 33:15-16)
Baraka juu ya familia
Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake. (Mithali 20:7)
Baraka ya furaha
Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai, lakini uadilifu huokoa kutoka mautini. (Mithali 10:2)
Baraka ya uzima
Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako. (Kumbukumbu 25:13-15)
Yeyote kati yenu anayependa uzima na kutamani kuziona siku nyingi njema, basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo. (Zaburi 34:12-13)
Midomo isemayo kweli hudumu milele, bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu. (Mithali 12:19)
Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi. (Ezekieli 33:14-16)
Baraka ya kuheshimiwa na watu
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako. Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu. (Mithali 3:3-4)
Baraka ya kufanikiwa
Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa, bali mapato ya waovu huwaletea taabu. (Mithali 15:6)
Baraka kwa viongozi
Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu. (Mithali 28:16)
Laana zilizowekwa kwa wadanganyifu
Laana ya kuchukiwa/kutengwa na Mungu
Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako. Kwa maana Bwana Mungu wako humchukia yeyote ambaye hufanya mambo kama haya, yeyote anayetenda kwa udanganyifu. (Kumbukumbu 25:13-16)
Unawaangamiza wasemao uongo. Bwana huwachukia wamwagao damu na wadanganyifu. (Zaburi 5:6)
...kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu, lakini siri yake iko kwa mwenye haki. (Mithali 3:32)
Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake: shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo, na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu. (Mithali 6:16, 19)
Bwana anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli. (Mithali 12:22)
Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo ataangamia. (Mithali 19:9)
Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa. (Isaya 57:17)
Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi na Mungu wenu, dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake, ili asisikie. Kwa maana mikono yenu imetiwa mawaa kwa damu na vidole vyenu kwa hatia. Midomo yenu imenena uongo, nazo ndimi zenu zimenongʼona mambo maovu. Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki; hakuna hata mmoja anayetetea shauri lake kwa haki. Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo, huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu. (Isaya 59:2-4)
Laana ya adhabu/hukumu
“Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.” (Kumbukumbu 27:17)
Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa. (Zaburi 63:11)
Bwana anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli. (Mithali 12:22)
Bwana huchukia sana mawazo ya mwovu, bali mawazo ya wale walio safi humfurahisha yeye. (Mithali 15:26)
Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo hataachwa huru. (Mithali 19:5)
Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe. (Mithali 20:17)
Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa. (Isaya 57:17)
Kama vitundu vilivyojaa ndege, nyumba zao zimejaa udanganyifu; wamekuwa matajiri na wenye nguvu, wamenenepa na kunawiri. Matendo yao maovu hayana kikomo; hawatetei mashauri ya yatima wapate kushinda, hawatetei haki za maskini. Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?” asema Bwana. “Je, nisijilipizie kisasi juu ya taifa kama hili? (Yeremia 5:27-29)
“Huweka tayari ndimi zao kama upinde, ili kurusha uongo; wamekuwa na nguvu katika nchi lakini si katika ukweli. Wanatoka dhambi moja hadi nyingine, hawanitambui mimi,” asema Bwana. “Jihadhari na rafiki zako; usiwaamini ndugu zako. Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu, na kila rafiki ni msingiziaji. Rafiki humdanganya rafiki, hakuna yeyote asemaye kweli. Wamefundisha ndimi zao kudanganya, wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi. Unakaa katikati ya udanganyifu; katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,” asema Bwana. Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu, kwani ni nini kingine niwezacho kufanya kwa sababu ya dhambi ya watu wangu? Ndimi zao ni mshale wenye sumu, hunena kwa udanganyifu. Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake, lakini moyoni mwake humtegea mtego. Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?” asema Bwana. “Je, nisijilipizie kisasi kwa taifa kama hili?” (Yeremia 9:3-9)
“ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi Bwana nimesema na nitalifanya. Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. (Ezekieli 22:13-15)
Maafisa wake walioko ndani yake ni kama mbwa mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu. Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo,’ wakati Bwana hajasema. Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki. “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, ambaye angejenga ukuta na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka kwa ajili ya watu wa nchi ili nisije nikaiangamiza, lakini sikumwona mtu yeyote. Hivyo nitaimwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwateketeza kwa moto wa hasira yangu, nikiyaleta juu ya vichwa vyao yale yote waliyotenda, asema Bwana Mwenyezi.” (Ezekieli 22:27-31)
Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji. (Hosea 5:10)
Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji, na kuwaonea maskini wa nchi, mkisema, “Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita ili tupate kuuza nafaka, na Sabato itakwisha lini ili tuweze kuuza ngano?” Mkipunguza vipimo, na kuongeza bei, na kudanganya kwa mizani zisizo sawa, mkiwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu, na mkiuza hata takataka za ngano pamoja na ngano. Bwana ameapa kwake mwenyewe, aliye Kiburi cha Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya. “Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili, nao wote waishio ndani mwake hawataomboleza? Nchi yote itainuka kama Naili; itapanda na kushuka kama mto wa Misri. “Katika siku ile,” asema Bwana Mwenyezi, “Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia iwe giza wakati wa mchana mwangavu. Nitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo, na kuimba kwenu kote kuwe kilio. Nitawafanya ninyi nyote mvae nguo ya gunia na kunyoa nywele zenu. Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. (Amosi 8:4-10)
Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu, hazina yako uliyopata kwa udanganyifu na vipimo vilivyopunguka, ambavyo vimelaaniwa? Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo? Matajiri wake ni wajeuri; watu wake ni waongo na ndimi zao zinazungumza kwa udanganyifu. Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu, kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu. Mtakula lakini hamtashiba; matumbo yenu bado yatakuwa matupu. Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote, kwa sababu mtakachoweka akiba nitatoa kwa upanga. Mtapanda lakini hamtavuna; mtakamua zeituni lakini hamtatumia mafuta yake. Mtakamua zabibu lakini hamtakunywa hiyo divai. Mmezishika sheria za Omri na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, tena umefuata desturi zao. Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi na watu wako kuwa dhihaka; mtachukua dharau za mataifa.” (Mika 6:10-16)
Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.” (Mathayo 21:12-13)
Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo. Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” (Luka 19:45-46)
Laana ya kifo/maangamizi
Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao. Yule atakayekutwa na vitu vilivyowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Bwana na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ” Yoshua akasema, “Kwa nini umeleta taabu hii juu yetu? Bwana ataleta taabu juu yako leo hii.” Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto. (Yoshua 7:11, 15, 25)
Unawaangamiza wasemao uongo. Bwana huwachukia wamwagao damu na wadanganyifu. (Zaburi 5:6)
Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli. Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila! Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka hema yako, atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai. (Zaburi 52:3-5)
Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye mali. (Mithali 1:19)
Mtu mbaya sana na mlaghai, ambaye huzungukazunguka na maneno ya upotovu, Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula; ataangamizwa mara, pasipo msaada. (Mithali 6:12, 15)
Midomo isemayo kweli hudumu milele, bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu. (Mithali 12:19)
Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha. (Mithali 21:6)
Yeye aupandaye uovu huvuna taabu, nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa. (Mithali 22:8)
Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini, wala kumdhulumu mhitaji mahakamani, kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao naye atawateka wao waliowateka. (Mithali 22:22-23)
“Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu katika mapato ya udhalimu, kwa kumwaga damu isiyo na hatia, kwa uonevu na ukatili.” Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: “Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, ndugu yangu! Ole, umbu langu!’ Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, bwana wangu! Ole, fahari yake!’ Atazikwa maziko ya punda: ataburutwa na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.” (Yeremia 22:17-19)
“Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya (ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya): “Hula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima. Humtia unajisi mke wa jirani yake. Huwaonea maskini na wahitaji. Hunyangʼanyana. Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake. Huziinulia sanamu macho. Hufanya mambo ya machukizo. Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Lakini baba yake atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe, kwa sababu alitoza bei isiyo halali kwa nguvu, akamnyangʼanya ndugu yake na kufanya yaliyo mabaya miongoni mwa watu wake. (Ezekieli 18:10-13, 18)
Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume. Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.” Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika. Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.” Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.” Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. (Matendo 5:1-10)
Laana juu ya familia
Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu, bali yeye achukiaye rushwa ataishi. (Mithali 15:27)
Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao, na mashamba yao kwa wamiliki wengine. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. (Yeremia 8:10)
Ole kwa wale wapangao uovu, kwa wale wafanyao shauri la hila vitandani mwao! Kunapopambazuka wanalitimiza kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza. Wanatamani mashamba na kuyakamata, pia nyumba na kuzichukua. Wanamlaghai mwanaume nyumba yake, mwanadamu mwenzake urithi wake. Kwa hiyo, Bwana asema: “Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa, ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe. Hamtatembea tena kwa majivuno, kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa. (Mika 2:1-3)
Laana juu ya mali
...hata hivyo baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru. Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi. (Mwanzo 31:7, 9)
Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai, lakini uadilifu huokoa kutoka mautini. (Mithali 10:2)
Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka. (Mithali 13:11)
Nyumba zao zitapewa watu wengine, pamoja na mashamba yao na wake zao, nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya wale waishio katika nchi,” asema Bwana. “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata faida zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. (Yeremia 6:12-13)
Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga, ndivyo alivyo mtu apataye mali kwa njia zisizo za haki. Maisha yake yafikapo katikati, siku zitamwacha, na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu. (Yeremia 17:11)
“Inuka upure, ee Binti Sayuni, kwa kuwa nitakupa pembe za chuma; nitakupa kwato za shaba na utavunja vipande vipande mataifa mengi.” Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Bwana, utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote. (Mika 4:13)
Laana ya kiburi
Yeye aupandaye uovu huvuna taabu, nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa. (Mithali 22:8)
Laana juu ya walio chini ya kiongozi
Kama mtawala akisikiliza uongo, maafisa wake wote huwa waovu. (Mithali 29:12)
Laana ya milele
Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.” (Ufunuo 21:8)
Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:27)
Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya. (Ufunuo 22:15)
Laana kwa ujumla
“Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.” (Kumbukumbu 27:17)
Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe. (Mithali 20:17)
Ole wa mji umwagao damu, uliojaa uongo, umejaa nyara, usiokosa kuwa na vitu vya kuteka nyara. (Nahumu 3:1)
Mtazamo wa watu kwamba Mungu haadhibu udanganyifu
“Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu? Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio? Watu husogeza mawe ya mpaka; huchunga makundi ya wanyama waliyonyangʼanya kwa nguvu. Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini, nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada. Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote kwa kutenda mabaya. (Ayubu 24:1-2, 12)
Rushwa
Watu hutoa rushwa
Rushwa hufanya kazi
Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; kokote kigeukiapo, hufanikiwa. (Mithali 17:8)
Zawadi itolewayo kwa siri hutuliza hasira na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali. (Mithali 21:14)
Waovu hutoa rushwa
Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wamwagao damu, ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa. (Zaburi 26:9-10)
Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri ili kupotosha njia ya haki. (Mithali 17:23)
Mifano ya waliotoa rushwa
Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki. (1 Samweli 8:3)
Watawala wenu ni waasi, rafiki wa wevi, wote wanapenda rushwa na kukimbilia hongo. Hawatetei yatima, shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe. (Isaya 1:23)
Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya, mtawala anadai zawadi, hakimu anapokea rushwa, wenye nguvu wanaamuru wanachotaka: wote wanafanya shauri baya pamoja. (Mika 7:3)
Wakati wale wanawake walikuwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo. (Mathayo 28:11-15)
Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.” Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye. (Matendo 24:25-26)
Amri ya kutoshiriki katika rushwa
“Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki. (Kutoka 23:8)
Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki. (Kumbukumbu 16:19)
Rushwa hupotosha
Dhuluma humfanya mtu mwenye hekima kuwa mpumbavu, nayo rushwa huuharibu moyo. (Mhubiri 7:7)
Mfano wa Bwana kutopokea rushwa
Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa. (Kumbukumbu 10:17)
Viongozi hawapaswi kupokea rushwa
Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu. Hukumuni kwa uangalifu, kwa kuwa kwa Bwana Mungu wetu hakuna jambo lisilo la haki, upendeleo, wala rushwa.” (2 Nyakati 19:7)
Kwa haki mfalme huipa nchi uthabiti, bali mfalme aliye na tamaa ya rushwa huiangamiza. (Mithali 29:4)
Mifano ya wasiopokea rushwa
Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni juu yangu mbele za Bwana na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Ni nani nimepata kumwonea? Ni kutoka kwenye mkono wa nani nimepokea rushwa ili kunifanya nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, mimi nitawarudishia.” Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutuonea. Hujapokea chochote kutoka kwenye mkono wa mtu awaye yote.” Samweli akawaambia, “Bwana ni shahidi juu yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.” Wakasema, “Yeye ni shahidi.” (1 Samweli 12:3-5)
Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu, au mnilipie fidia kutoka mali zenu, (Ayubu 6:22)
Baraka na laana
Wanaotoa rushwa wamelaaniwa
“Alaaniwe mtu apokeaye rushwa ili kumuua mtu asiye na hatia.” (Kumbukumbu 27:25)
...wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo, lakini huwanyima haki wasio na hatia. (Isaya 5:23)
Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa jirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema Bwana Mwenyezi. “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi Bwana nimesema na nitalifanya. Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. (Ezekieli 22:12-15)
Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake. Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani. (Amosi 5:11-12)
Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa, na makuhani wake wanafundisha kwa malipo, nao manabii wake wanatabiri kwa fedha. Hata hivyo wanamwegemea Bwana na kusema, “Je, Bwana si yumo miongoni mwetu? Hakuna maafa yatakayotupata.” Kwa hiyo kwa sababu yenu, Sayuni italimwa kama shamba, Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto, na kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu kilichofunikwa na vichaka. (Mika 3:11-12)
Wasiotoa rushwa wamebarikiwa
Zaburi ya Daudi. Bwana, ni nani awezaye kukaa katika Hekalu lako? Nani awezaye kuishi katika mlima wako mtakatifu? Yeye akopeshaye fedha yake bila riba, na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia. Mtu afanyaye haya kamwe hatatikisika. (Zaburi 15:1, 5)
Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu, bali yeye achukiaye rushwa ataishi. (Mithali 15:27)
Yeye aendaye kwa uadilifu na kusema lililo haki, yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma na kuizuia mikono yake isipokee rushwa, yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji, na yeye afumbaye macho yake yasitazame sana uovu: huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu, ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani. Atapewa mkate wake, na maji yake hayatakoma. (Isaya 33:15-16)