Amri ya kutotamani
Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.” (Kutoka 20:17)
Usitamani mke wa jirani yako. Usitamani nyumba ya jirani yako au shamba lake, mtumishi wake wa kiume au wa kike, ngʼombe au punda wake, wala kitu chochote cha jirani yako.” (Kumbukumbu 5:21)
Vinyago vya miungu yao mtavichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala msizichukue kwa ajili yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa navyo. Kwa kuwa ni chukizo kwa Bwana Mungu wenu. (Kumbukumbu 7:25)
Adhabu iliyoonywa kwa ajili ya tamaa
Lakini mjiepushe na vitu vilivyowekwa wakfu, msije mkachukua chochote katika hivyo, msije mkajiletea maangamizi katika maskani ya Israeli na kuiletea taabu. (Yoshua 6:18)
Ole kwa wale wapangao uovu, kwa wale wafanyao shauri la hila vitandani mwao! Kunapopambazuka wanalitimiza kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza. Wanatamani mashamba na kuyakamata, pia nyumba na kuzichukua. Wanamlaghai mwanaume nyumba yake, mwanadamu mwenzake urithi wake. Kwa hiyo, Bwana asema: “Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa, ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe. Hamtatembea tena kwa majivuno, kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa. (Mika 2:1-3)
Mfano wa adhabu kwa ajili ya tamaa
Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao. Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi. “Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kitu kilichowekwa wakfu kipo katikati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu mpaka mtakapokiondoa. “ ‘Asubuhi, mjihudhurishe kabila kwa kabila. Itakuwa kabila lile atakalolitwaa Bwana litakuja mbele ukoo kwa ukoo, ukoo ule atakaoutwaa Bwana utakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakuja mbele mtu kwa mtu. Yule atakayekutwa na vitu vilivyowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Bwana na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ” Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akawaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na Yuda akatwaliwa. Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawatwaa Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikatwaliwa. Yoshua akaamuru watu wa jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akatwaliwa. Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.” Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya: Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.” Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakapiga mbio mpaka hemani, tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, pamoja na ile fedha chini yake. Wakavichukua vile vitu toka mle hemani, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, na wakavitandaza mbele za Bwana. Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe na binti zake, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori. Yoshua akasema, “Kwa nini umeleta taabu hii juu yetu? Bwana ataleta taabu juu yako leo hii.” Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto. (Yoshua 7:11-25)
Mifano ya tamaa iliyotolewa ili kutufundisha
Basi mambo haya yalitokea kama mifano ili kutuzuia tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya. (1 Wakorintho 10:6)
Wenye tamaa hawataurithi Ufalme wa Mungu
Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. (1 Wakorintho 6:9-10)
Mtu mwenye tamaa ni mwabudu sanamu
Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu. (Waefeso 5:3)
Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. (Waefeso 5:5)
Usishirikiane na mwamini mwenye tamaa
Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi. Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyangʼanyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu. Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye. (1 Wakorintho 5:9-11)
Mfano wa mtu anayemcha Mungu asiyetamani
Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote. (Matendo 20:33)
Mungu anaweza kudhibiti tamaa
Mara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele za Bwana Mwenyezi, Mungu wa Israeli. Nitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yako wakati unapokwenda mara tatu kila mwaka kuonana na Bwana Mungu wako. (Kutoka 34:23-24)
Tamaa imetumika kama kielelezo cha kazi ya sheria
Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini, isingekuwa kwa sababu ya sheria, nisingalijua dhambi. Nisingalijua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.” Lakini dhambi kwa kupata nafasi katika amri, hii ikazaa ndani yangu kila aina ya tamaa. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa. (Warumi 7:7-8)