Je, kuweka akiba/kuwekeza ni halali kwa mujibu wa Maandiko?
Mistari inayoonekana kukataza kuweka akiba
“Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa. (Mathayo 6:19-21)
“Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali. “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. (Mathayo 6:24-33)
Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.” Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.” Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?” Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” (Mathayo 19:16-21)
Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. (Marko 6:8)
Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata. (Luka 5:11)
Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine? “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia. “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia. (Luka 12:22-34)
Mtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ” Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.” Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.” Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!” Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.” (Luka 18:18-30)
Tunaweza kuweka akiba na kuwekeza tu ikiwa tunatoa pia
Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.” Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.” Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’ “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’ “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’ “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.” (Luka 12:13-21)
Mfano unaotumia kuweka akiba na kuwekeza
“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao. Mmoja akampa talanta tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri. Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi. Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi. Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake. “Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao. Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’ “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’ “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’ “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’ “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu. Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’ “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu. Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake. “ ‘Basi mnyangʼanyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi. (Mathayo 25:14-28)
Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi. Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake, na akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi mpaka nitakaporudi.’ “Lakini raiya wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’ “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara. “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia, nimepata faida mara kumi zaidi.’ “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’ “Wa pili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’ “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’ “Kisha akaja yule mtumishi mwingine, akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa. Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka kitu, na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’ “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna mahali ambapo sikupanda, kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba, ili nitakaporudi nichukue iliyo yangu na riba yake?’ “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyangʼanyeni fungu lake la fedha, mkampe yule mwenye kumi.’ (Luka 19:12-24)
Malengo ya uwekezaji
Malengo ya uwekezaji yanayokubalika
Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini. (1 Timotheo 5:8)
Kuacha urithi
Ni sahihi kuacha urithi
Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki. (Mithali 13:22)
Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana. (Mithali 19:14)
Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.” (Isaya 38:1)
Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara hii ya tatu, nami sitawalemea, kwa sababu sitahitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi, kwa kuwa hata hivyo watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. (2 Wakorintho 12:14)
Sheria za Agano la Kale kuhusu urithi
Hao waweza kuwarithisha watoto wako kuwa urithi wao, na wanaweza kuwafanya watumwa maisha yao yote, lakini usiwatawale ndugu zako Waisraeli kwa ukatili. (Walawi 25:46)
“Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake. Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake. Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake. Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama Bwana alivyomwamuru Mose.’ ” (Hesabu 27:8-11)
Wakasema, “Bwana alipomwamuru bwana wangu kuwapa Waisraeli nchi kama urithi kwa kura, alikuamuru kutoa urithi wa ndugu yetu Selofehadi kwa binti zake. Sasa ikiwa wataolewa na watu wa makabila mengine ya Kiisraeli, itakuwa kwamba urithi wao utaondolewa kutoka urithi wa mababu zetu na kuongezwa katika urithi wa kabila ambalo dada hao wameolewa. Kwa hiyo sehemu ya urithi tuliyogawiwa itachukuliwa kutoka kwetu. Wakati mwaka wa Yubile kwa Waisraeli utafika, urithi wao utaongezwa kwa lile kabila ambalo wameolewa, na mali yao itaondolewa kutoka urithi wa kabila la mababu zetu.” Ndipo kwa agizo la Bwana Mose akatoa amri ifuatayo kwa Waisraeli: “Kile wazao wa kabila la Yosefu wanachosema ni kweli. Hivi ndivyo Bwana anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu yeyote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila za baba yao. Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake. Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lolote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake. Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.” (Hesabu 36:2-9)
Atashiriki sawa katika mafao yao, hata kama amepokea fedha kutoka mauzo ya mali ya jamaa yake. (Kumbukumbu 18:8)
Kama mwanaume ana wake wawili, naye anampenda mmoja na mwingine hampendi na wote wawili wamemzalia wana wa kiume, lakini mwana mzaliwa wa kwanza ni wa yule mke asiyempenda, wakati anapotoa wosia wa mali yake kwa wanawe, kamwe asitoe haki za mzaliwa wa kwanza kwa mwana wa mke ampendaye kwa upendeleo, badala ya mzaliwa hasa wa kwanza, ambaye ni mwana wa mke ambaye hampendi. Ni lazima amkubali mwana wa mke asiyempenda kama mzaliwa wa kwanza kwa kumpa sehemu ya vile vyote alivyo navyo maradufu. Mwana huyo ni ishara ya kwanza ya nguvu za baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye. (Kumbukumbu 21:15-17)
“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ikiwa mkuu atawalaye atatoa zawadi kutoka kwenye urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake, itakuwa mali yao kwa urithi. Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka mpaka mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao. Mkuu anayetawala hana ruhusa kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali zao. Mkuu atawalaye atawapa wanawe urithi wao, kutoka kwenye mali zake mwenyewe, ili kwamba pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ” (Ezekieli 46:16-18)
Bwana na zaka vilikuwa urithi wa Walawi
Bwana akamwambia Aroni, “Hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli. “Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania. Kuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa. Ni Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wowote miongoni mwa Waisraeli. Badala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwa Bwana kuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuhusu wao: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ” (Hesabu 18:20-24)
“ ‘Mimi nitakuwa ndio urithi pekee walio nao makuhani katika Israeli. Msiwape wao milki, mimi nitakuwa milki yao. Wao watakula sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia na kila kitu kitakachotolewa kwa Bwana katika Israeli kitakuwa chao. Yote yaliyo bora ya malimbuko ya vitu vyote na matoleo yenu maalum vitakuwa vya makuhani. Inawapasa kuwapa malimbuko ya kwanza ya unga wenu ili kwamba baraka ipate kuwa katika nyumba zenu. (Ezekieli 44:28-30)
Mifano ya kuacha urithi
Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina hata mtoto na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.” Ndipo neno la Bwana lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” (Mwanzo 15:2-4)
Bwana amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda. Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho. (Mwanzo 24:35-36)
Abrahamu akamwachia Isaki kila kitu alichokuwa nacho. (Mwanzo 25:5)
Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tu tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu? Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata na vile vilivyolipwa kwa ajili yetu. Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.” (Mwanzo 31:14-16)
Ndipo Israeli akamwambia Yosefu, “Mimi ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.” (Mwanzo 48:21-22)
Nayo ile mifupa ya Yosefu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo, ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yosefu. (Yoshua 24:32)
Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.” Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.” (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.) Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake. Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni. Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!” (Ruthu 4:5-10)
Baba yao alikuwa amewapa zawadi nyingi za fedha na dhahabu na vitu vya thamani, pamoja na miji yenye ngome huko Yuda, bali ufalme akampa Yehoramu kwa sababu alikuwa mwanawe mzaliwa wa kwanza. (2 Nyakati 21:3)
Nimeshaona uovu mzito chini ya jua: Utajiri uliolimbikizwa kwa kujinyima na kuleta madhara kwa mwenye mali, au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya, hivyo kwamba wakati akiwa na mwana hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake. (Mhubiri 5:13-14)
Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema na huwafaidia wale walionalo jua. (Mhubiri 7:11)
Baraka moja ya utii wa kumcha Mungu ilikuwa uwezo wa kuacha na kupokea urithi
“Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Bwana naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Bwana Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele. (1 Nyakati 28:8)
Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’ (Ezra 9:12)
Ni nani basi, mtu yule anayemcha Bwana? Atamfundisha katika njia atakayoichagua kwa ajili yake. Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake, nao wazao wake watairithi nchi. (Zaburi 25:12-13)
Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu. (Mithali 17:2)
Mfano unaotumia kielelezo cha kuweka akiba na kuwekeza
Yesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake. “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote. Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote. “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake. “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu. “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’ “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija. “Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza. Akamwita mmoja wa watumishi na kumuuliza, ‘Kuna nini?’ Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’ “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumsihi. Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana-mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu. Lakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’ “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako. (Luka 15:11-31)
Yesu anajibu swali kuhusu urithi
Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.” Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.” (Luka 12:13-15)
Urithi unaotolewa mapema mno hautakuwa baraka
Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni. (Mithali 20:21)
Ilikuwa desturi kumteua mlezi hadi mrithi atakapokuwa na umri wa kusimamia mali
Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake. (Wagalatia 4:1-2)
Ni ubatili kufanya kazi kwa bidii ili kumwachia mpumbavu urithi au wakati huna mrithi
Nikachukia kila kitu nilichokuwa nimetaabikia chini ya jua, kwa sababu ni lazima nimwachie yule ajaye baada yangu. Nani ajuaye kama atakuwa ni mtu mwenye hekima au mpumbavu? Lakini hata hivyo yeye ndiye atakayetawala kazi zote ambazo nimemiminia juhudi na ustadi chini ya jua. Hili nalo ni ubatili. Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi yangu yote niliyoifanya kwa taabu chini ya jua. Kwa kuwa mtu anaweza kufanya kazi yake kwa hekima, maarifa na ustadi, kisha analazimika kuacha vyote alivyo navyo kwa mtu mwingine ambaye hajavifanyia kazi. Hili nalo pia ni ubatili tena ni balaa kubwa. (Mhubiri 2:18-21)
Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake, hakuwa na mwana wala ndugu. Hapakuwa na mwisho wa kazi yake, hata hivyo macho yake hayakutosheka na utajiri wake. Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani, nami kwa nini ninajinyima kufurahia?” Hili pia ni ubatili, ni shughuli yenye taabu! (Mhubiri 4:8)
Malengo ya uwekezaji yasiyokubalika
Tamaa ya kutajirika
Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. (1 Timotheo 6:9)
Tunapotamani kutajirika, tunapenda fedha
Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi. (1 Timotheo 6:10)
Ikimbie tamaa ya kutajirika
Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. (1 Timotheo 6:11)
Mwabudu Bwana peke yake
Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.” Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ” (Mathayo 4:8-10)
Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja. Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ” (Luka 4:5-8)
Kuweka akiba
Katika nyumba ya mwenye hekima kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta, lakini mtu mpumbavu hutafuna vyote alivyo navyo. (Mithali 21:20)
“Vitu vinne duniani vilivyo vidogo, lakini vina akili nyingi sana: Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo, hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi. (Mithali 30:24-25)
Mfano wa kuweka akiba kwa ajili ya mahitaji ya baadaye
Farao na aweke wenye amri nchini kote wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya neema. Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.” (Mwanzo 41:34-36)
Mfumo wa Mungu wa uwekezaji wenye mafanikio
Jua Bwana anataka uwekeze wapi
Hili ndilo asemalo Bwana, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea. (Isaya 48:17)
Gawanya uwekezaji wako
Wape sehemu watu saba, naam hata wanane, kwa maana hujui ni baa gani litakalokuwa juu ya nchi. (Mhubiri 11:2)
Biashara/kazi kabla ya kupata nyumba
Maliza kazi zako za nje, nawe uweke mashamba yako tayari, baada ya hayo, jenga nyumba yako. (Mithali 24:27)
Wale waliomiliki nyumba
Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. (Mathayo 8:14)
Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. (Marko 1:29)
Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie. (Luka 4:38)
Wale wasiomiliki nyumba
Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.” (Mathayo 8:20)
Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwa nyumba aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote waliokwenda kumwona. (Matendo 28:30)
Epuka uwekezaji wenye hatari
Nimeshaona uovu mzito chini ya jua: Utajiri uliolimbikizwa kwa kujinyima na kuleta madhara kwa mwenye mali, au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya, hivyo kwamba wakati akiwa na mwana hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake. (Mhubiri 5:13-14)
Hili nalo ni baya la kusikitisha: Kama vile mtu ajavyo, vivyo hivyo huondoka, naye anapata faida gani, maadamu hutaabika kwa ajili ya upepo? (Mhubiri 5:16)
Kuwa mfanyakazi wa kudumu
Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini. (Mithali 21:5)
Usiwe na haraka
Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini. (Mithali 21:5)
Mtu mwaminifu atabarikiwa sana, bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka hataacha kuadhibiwa. (Mithali 28:20)
Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri, naye hana habari kuwa umaskini unamngojea. (Mithali 28:22)
Wakati sahihi ni muhimu
Kuna wakati kwa ajili ya kila jambo, nayo majira kwa kila tendo chini ya mbingu: (Mhubiri 3:1)
Jua hali ya kifedha ili kukidhi mahitaji na kutimiza malengo
Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako ya kondoo na mbuzi, angalia kwa bidii ngʼombe zako. Kwa kuwa utajiri haudumu milele, nayo taji haidumu vizazi vyote. Wakati majani makavu yameondolewa na mapya yamechipua, nayo majani toka milimani yamekusanywa, wana-kondoo watakupatia mavazi na mbuzi thamani ya shamba. Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi kukulisha wewe na jamaa yako, na kuwalisha watumishi wako wa kike. (Mithali 27:23-27)
“Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, (Luka 14:28-29)
Kupanga na utaratibu kunahimizwa
Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo. (Mithali 20:18)
Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini. (Mithali 21:5)
Kwa hekima nyumba hujengwa, nayo kwa njia ya ufahamu huimarishwa kwa njia ya maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza. (Mithali 24:3-4)
Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu. (1 Wakorintho 14:40)
Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani. Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu, (1 Wakorintho 14:33)
Maagizo kwa wawekezaji wenye mafanikio
Usiwe na kiburi
Hili ndilo asemalo Bwana: “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake, au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake, wala tajiri ajisifu katika utajiri wake, lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili: kwamba ananifahamu na kunijua mimi, kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema, hukumu na haki duniani, kwa kuwa napendezwa na haya,” asema Bwana. (Yeremia 9:23-24)
Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. (1 Timotheo 6:17)
Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. Kwa maana jua kali lenye kuchoma huchomoza na kuliunguza, likayakausha majani, na ua lake likapukutika, nao uzuri wake huharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake. (Yakobo 1:9-11)
Usiutumainie utajiri
Kwa kuwa mmetumainia matendo yenu na mali zenu, ninyi pia mtachukuliwa mateka, naye Kemoshi atakwenda uhamishoni, pamoja na makuhani wake na maafisa wake. (Yeremia 48:7)
Kwa nini unajivunia mabonde yako, kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana? Ee binti usiye mwaminifu, unayeutumainia utajiri wako na kusema, ‘Ni nani atakayenishambulia?’ Nitaleta hofu kuu juu yako kutoka kwa wale wote wanaokuzunguka,” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Kila mmoja wenu ataondolewa, wala hakuna hata mmoja atakayekusanya wakimbizi. (Yeremia 49:4-5)
Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. (1 Timotheo 6:17)
Toa kwa ukarimu
Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. (1 Timotheo 6:18)
Usiwe mtu asiyefikika
Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi. (Isaya 5:8)
Kanuni za jumla za uwekezaji
Lipa bei ya haki kwa uwekezaji
“ ‘Ikiwa utauza ardhi kwa mmoja wa wazawa wa nchi yako, au ukinunua ardhi kutoka kwake, mmoja asimpunje mwingine. Utanunua ardhi kwa mzawa wa nchi yako kwa misingi ya hesabu ya miaka baada ya Yubile. Naye ataiuza kwako kwa misingi ya hesabu ya miaka iliyobaki kwa kuvuna mavuno. Miaka inapokuwa mingi, utaongeza bei, nayo miaka ikiwa michache, utapunguza bei, kwa sababu kile anachokuuzia kwa hakika ni hesabu ya mazao. Mmoja asimpunje mwingine, bali utamcha Mungu wako. Mimi ndimi Bwana Mungu wako. (Walawi 25:14-17)
Wengine hudanganya ili wasilipe bei ya haki
“Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake. (Mithali 20:14)
Inakubalika mke kuwekeza
Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata? Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani. (Mithali 31:10)
Huangalia shamba na kulinunua, kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu. (Mithali 31:16)
Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, naye huwauzia wafanyabiashara mishipi. (Mithali 31:24)
Kukopesha
Mwamini wa Agano la Kale alipaswa kuwakopesha waamini wenye mahitaji
Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. (Kumbukumbu 15:7-9)
Mkopeshaji alibarikiwa
Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba, anayefanya mambo yake kwa haki. (Zaburi 112:5)
Agano Jipya lilipanua wajibu kwa wale walioomba mkopo
Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa. (Mathayo 5:42)
Riba haikupaswa kutozwa
“Kama ukimkopesha mmojawapo wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. (Kutoka 22:25)
“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida. (Walawi 25:35-37)
Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine chochote ambacho waweza kupata riba juu yake. (Kumbukumbu 23:19)
Mfano wa kuvunja sheria hii
Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.” Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu. Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu na binti zetu kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya wengine.” Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana. Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaitisha mkutano mkubwa ili kuwashughulikia na kusema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wasioamini. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Walinyamaza kimya, kwa sababu hawakupata chochote cha kusema. Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu wasioamini? Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome! Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.” Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu chochote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.” Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi. (Nehemia 5:3-12)
Amebarikiwa asipotoza riba
Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili kwamba Bwana Mungu wako akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki. (Kumbukumbu 23:20)
Zaburi ya Daudi. Bwana, ni nani awezaye kukaa katika Hekalu lako? Nani awezaye kuishi katika mlima wako mtakatifu? Yeye akopeshaye fedha yake bila riba, na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia. Mtu afanyaye haya kamwe hatatikisika. (Zaburi 15:1, 5)
Hamwonei mtu yeyote, bali hurudisha kilichowekwa rehani kwake. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi. Hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huuzuia mkono wake usifanye mabaya, naye huhukumu kwa haki kati ya mtu na mtu. Huzifuata amri zangu na kuzishika sheria zangu kwa uaminifu. Huyo mtu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mwenyezi. “Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya (ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya): “Hula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima. Humtia unajisi mke wa jirani yake. Huwaonea maskini na wahitaji. Hunyangʼanyana. Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake. Huziinulia sanamu macho. Hufanya mambo ya machukizo. Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. “Lakini yawezekana mwana huyo ana mwana aonaye dhambi hizi zote anazofanya baba yake, naye ingawa anaziona, yeye hafanyi mabaya kama haya: “Hakula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima, wala hainulii macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake. Hakumwonea mtu yeyote wala hakutaka rehani kwa ajili ya mkopo. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi. Huuzuia mkono wake usitende dhambi, hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huzishika amri zangu na kuzifuata sheria zangu. Hatakufa kwa ajili ya dhambi za baba yake; hakika ataishi. (Ezekieli 18:7-17)
Amelaaniwa akitoza riba
Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno hukusanya kwa ajili ya mwingine, ambaye atawahurumia maskini. (Mithali 28:8)
“Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. (Ezekieli 18:10, 13)
Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa jirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema Bwana Mwenyezi. “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. (Ezekieli 22:12-13)
“Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema, “ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu! Ataendelea hivi kwa muda gani?’ Je, wadai wako hawatainuka ghafula? Je, hawataamka na kukufanya utetemeke? Kisha utakuwa mhanga kwao. (Habakuki 2:6-7)
Iliruhusiwa kumtoza mgeni riba
Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili kwamba Bwana Mungu wako akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki. (Kumbukumbu 23:20)
Kitu cha lazima hakikupaswa kuchukuliwa kama rehani ya mkopo
Kama ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma. (Kutoka 22:26-27)
Usitoe jozi ya mawe ya kusagia, hata ikiwa lile la juu, kuweka rehani kwa ajili ya deni, kwa sababu itakuwa ni kuweka uhai wa mtu kama dhamana. Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani kwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Bwana Mungu wako. (Kumbukumbu 24:6, 10-13)
Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. (Kumbukumbu 24:17)
Shutuma ya kuvunja sheria hii
Je, uovu wako si mkuu? Dhambi zako si hazina mwisho? Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu; umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi. (Ayubu 22:5-6)
Amebarikiwa asipochukua rehani ya namna hiyo
Hamwonei mtu yeyote, bali hurudisha kilichowekwa rehani kwake. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi. Huzifuata amri zangu na kuzishika sheria zangu kwa uaminifu. Huyo mtu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mwenyezi. Hakumwonea mtu yeyote wala hakutaka rehani kwa ajili ya mkopo. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi. Huuzuia mkono wake usitende dhambi, hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huzishika amri zangu na kuzifuata sheria zangu. Hatakufa kwa ajili ya dhambi za baba yake; hakika ataishi. (Ezekieli 18:7, 9, 16-17)
...kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. (Ezekieli 33:15)
Amelaaniwa akichukua rehani ya namna hiyo
“Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya Huwaonea maskini na wahitaji. Hunyangʼanyana. Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake. Huziinulia sanamu macho. Hufanya mambo ya machukizo. Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. (Ezekieli 18:10, 12-13)
Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Israeli, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Wanawauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu. Watu hulala kando ya kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani. Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu. (Amosi 2:6, 8)
Waovu huchukua rehani za namna hiyo
Huwanyangʼanya yatima punda wao, na kumchukua rehani fahali wa mjane. Mtoto yatima hupokonywa matitini; mtoto wachanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni. (Ayubu 24:3, 9)
Kulipa mkopo hakukudaiwa
Huwanyangʼanya yatima punda wao, na kumchukua rehani fahali wa mjane. Mtoto yatima hupokonywa matitini; mtoto wachanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni. (Ayubu 24:3, 9)
Madeni yalisamehewa kila miaka saba
Katika Agano Jipya, wakopesheni hata adui bila kutarajia kurudishiwa
Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. (Luka 6:34-35)