Amri ya kutoabudu sanamu
Msijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu. (Kutoka 20:23)
Sanamu ni kazi ya mikono ya watu
Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. (Zaburi 115:4)
Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. (Zaburi 135:15)
Mungu hutoa kila kitu, hata vifaa vinavyotumiwa kutengeneza sanamu
Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta, niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia kwa kumtumikia Baali. (Hosea 2:8)
Nitamwadhibu kwa ajili ya siku alizowafukizia uvumba Mabaali; alipojipamba kwa pete na kwa vito vya thamani, na kuwaendea wapenzi wake, lakini mimi alinisahau,” asema Bwana. (Hosea 2:13)
Choyo kinalinganishwa na ibada ya sanamu
Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. (Wakolosai 3:5)
Mungu huwahukumu wanaoabudu sanamu
Watakushughulikia kwa chuki na kukunyangʼanya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao. (Ezekieli 23:29-30)
Sanamu zake zote zitavunjwa vipande vipande; zawadi zake zote za Hekalu zitachomwa kwa moto; nitaharibu vinyago vyake vyote. Kwa kuwa alikusanya zawadi zake kutokana na ujira wa kahaba, nazo zitatumika tena kulipa mishahara ya kahaba.” (Mika 1:7)
Mfano wa watu wa Mungu kuharibu sanamu, kisha Bwana akawabariki
Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!” Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. (Isaya 30:22-23)
Mfano wa ibada ya sanamu iliyofichwa ndani ya dini
Akamwambia mama yake, “Zile shekeli 1,100 za fedha zilizochukuliwa kwako, ambazo nilisikia ukizinenea maneno ya laana, hizi hapa; mimi ndiye niliyezichukua, lakini sasa ninakurudishia.” Ndipo mama yake akamwambia, “Bwana na akubariki, mwanangu.” Alipozirudisha zile shekeli 1,100 za fedha kwa mama yake, mama yake akamwambia, “Mimi nimeiweka fedha hii wakfu kwa Bwana kwa ajili ya mwanangu kutengenezea kinyago cha kuchonga na sanamu ya kusubu. Mimi nitakurudishia wewe.” Hivyo akamrudishia mama yake ile fedha, naye mama yake akachukua shekeli mia mbili za hiyo fedha na kumpa mfua fedha, ambaye aliifanyiza kinyago na sanamu. Navyo vikawekwa ndani ya nyumba ya Mika. (Waamuzi 17:2-4)